Benki ya CRDB yatoa msaada wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa shule za msingi Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda (kushoto) na mwanafunzi(katikati)

Dar es Salaam Tanzania, Juni 14, 2015 – Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa shilingi milioni 100 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa shule za msingi na sekondari, ikiwa ni moja ya sehemu ya Benki hiyo katika kuisaidia jamii. Kwa kuzingatia mahitaji ya jamii inayoizunguka, Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kusaidia jamii ambayo inalenga kurudisha kiasi cha asilimia moja ya faida ya Benki hiyo kila mwaka, ili ziende katika shughuli za kijamii, hususani katika nyanja za elimu, afya na mazingira.

Akizungumza katika makabidhiano hayo ambayo yalihudhuriwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam Ndugu. Issa Mwita pamoja na Mameya na Wakuu wa Wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya elimu nchini na ndio maana elimu imepewa umuhimu mkubwa katika sera yetu ya kuisaidia jamii. Tunatambua kuwa ili taifa letu liweze kupiga hatua za kimaendeleo, ni lazima tuwekeze katika kuboresha sera na miundo mbinu ya elimu ili kuzalisha rasilimali watu ya kutosheleza mahitaji ya taifa letu.” Dkt alisema Benki ya CRDB ikiwa kama mdau wa maendeleo inatambua kuwa juhudi za wananchi katika kujikwamua katika umaskini hazitafanikiwa kama taifa litashindwa kutoa elimu iliyo bora kwa wananchi wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda

Dkt. Kimei alisema kupitia sera ya msaada kwa jamii, Benki ya CRDB imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika sekta ya elimu na imekuwa ikielekeza nguvu katika kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maktaba, matundu ya vyoo, vitabu pamoja na vifaa mbalimbali vya kufundishia. Benki ya CRDB pia imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na Taasisi ya Elimu nchini (TEA) katika kuchangia maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu ambapo kila mwaka benki hiyo imekuwa ikichangia kiasi cha shilingi milioni 20 ili kuisaidia taasisi hiyo kuweza kutimiza majukumu yake kwa ufasaha.

“Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa kuchangia ujenzi, upanuzi na uboreshaji wa vyuo vikuu nchini ambapo pamoja na mambo mengine, benki pia imekuwa ikitoa nafasi za mafunzo ya kazi “field and internship” kwa wanafunzi zaidi ya 5,000 kila mwaka ili kuwajenga uzoefu wa kazi.” Alisema Dkt. Kimei.

Dkt. Kimei alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa ikizikumba shule za msingi na sekondari hususani katika upande wa madawati, viti na meza, huku akiwahakikishia ya kuwa Benki hiyo iko nao bega kwa bega kwatika kuhakikisha kuwa mazingira ya elimu nchini yanaboreka.

“Tunaamini kuwa mchango huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo sugu mkoani Dar es salaam na kusema kuwa huu ni mwanzo tu, Inshallah tutaendelea kusaidia mpaka siku moja kuona kuwa kila mtoto anakaa kwemye dawati. Si hapa Dar es Salaam tu, bali Tanzania nzima.” Alisema Dkt. Kimei.

Msaada huo wa fedha ambao unategemewa kufanikisha ununuzi wa jumla ya madawati 1,500 ni moja ya misaada mingi ambayo Benki ya CRDB imeitoa kwa jamii kwa kipindi cha mwaka huu ikiwa inasherehekea miaka 20 tokea kuanzishwa kwake. “Mwaka huu tuliweka dhamira ya kuisaidia jamii zaidi ikiwa ni sehemu ya kuwashukuru wateja wetu kwa kuifanya Benki ya CRDB kuwa benki chaguo nambari moja.” Alisema Dkt. Kimei

Dkt. Kimei alisema kwa mwaka huu Benki ya CRDB imekuwa ikijikita zaidi katika kusaidia elimu ikiwa ni harakati za kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi John Pombe Magufuli husuani filosofia yake ya kutoa elimu bora kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule. Filosofia ambayo imeshaanza kutekelezwa kwa vitendo, ambayo benki hiyo ina amini ndio njia bora zaidi ya kuifikia Tanzania huru na yenye maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda aliipongeza Benki ya CRDB akisema kuwa Benki hiyo imekuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine katika nyanja mbalimbali, huku akiishukuru benki hiyo kwa msaada huo wa shilingi milioni 100 akisema msaada huo utakwenda kuwasaidia zaidi ya wanafunzi 4,500 katika jiji la Dar es Salaam ambao walikuwa wakikaa chini kutokana na ukosefu wa madawati. “Msaada huu unatupa faraja kubwa sana ya kuwa wapo watanzania na taasisi zinazoguswa na maendeleo ya elimu nchini, naomba nikuhakikishie ya kuwa msaada huu utaenda kufanya kazi iliyokusudiwa na naomba wadau wengine wajitokeze na kuiga mfano huu ulioonyeshwa na Benki ya CRDB.” Alisema Mh. Paul Makonda.

Dkt. Kimei alimalizia hotuba yake kwa kuwa kuwasihi wadau wote wa elimu nchini waweze kuunga jitihada hizo katika kuinua viwango vya elimu kwa kutoa michango yao ya hali na mali. “Wito huu si kwa taasisi tu bali hata wananchi na watu binafsi kwani kama waswahili wasemavyo “haba na haba hujaza kibaba”.” alisema Dkt. Kimei.

Ili kuwapa fursa na wadau wengine waweze kutoa michango yao kwa urahisi uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umefungua akaunti maalumu ya uchangiaji wa madawati kupitia benki ya CRDB yenye nambari “0113941800” katika tawi la Benki ya CRDB pale Kijitonyama. Akaunti ambayo inalenga kuwapa fursa wadau wote kuchangia katika kampeni hii maalum ya ununuaji wa madawati.

“Kufungua akaunti maalum kwa ajili ya uchangia wa elimu ni jambo muhimu na la kuponezwa, hii itasaidia kuwapa nafasi wadau wengine kutoa michango yao pale walipo. Hivyo napenda kuwajulisha wadau wote kutumia fursa hii kuchangia kupitia njia zetu mbalimbali za huduma ikiwemo kupitia simu zao za mikononi yaani Simbaking, Wakala wetu wa FahariHuduma au kupitia tawi lolote la Benki ya CRDB nchini.” alimalizia Dkt. Kimei.

-MWISHO-

Kuhusu Benki ya CRDB

Benki ya CRDB ilianzishwa mwaka 1996 na imeendelea kukua zaidi hadi kufikia kuwa benki inayoaminika, chaguo la kwanza la mteja na kuongoza kwa ubanifu katika soko. Benki ya CRDB imekuwa ikirekodi ongezeko la faida kila mwaka tokea ilipoanzishwa na imekuwa ikilipa gawio kila mwaka kwa wanahisa wake. Benki ilipiga hatua muhimu hivi karibuni baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuanzisha kampuni tanzu ya CDRB Burundi.

Benki ya CRDB inatoa huduma mbalimbali kwa wateja wakubwa, wakati na wadogo kupitia matawi zaidi ya 198, Matawi yanayo tembea 12, Mashine za kutolea hela zaidi ya 461, Mashine za kuweka hela 15, vifaa vya manunuzi (PoS) zaidi ya 1,500 na Mawakala wa FahariHuduma zaidi ya 1,769. Pia Benki ya CDRB inatoa huduma ya kibenki kupitia mtandao “Internet banking” na huduma ya kibenki kupitia simu ya mkononi ijulikanayo kama SimBanking.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Jina Namba ya Simu Barua Pepe
Tully Esther Mwambapa +255 769 200 600

This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu +254 784 002 020 This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);