CRDB Bank yazindua kituo cha kisasa cha kutolea huduma “Premier Club” pamoja na kadi ya kimataifa ya TemboCardVisa Infinite

Dar Es Salaam Tanzania, September 02, 2016 – Benki ya CRDB leo imezindua kituo cha kisasa kwa ajili ya kuwahudumia wateja wakubwa kijulikanacho kama “Premier Club” pamoja na kadi mpya yenye viwango vya kimataifa ya TemboCardVisa Infinite katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Serena iliyopo katikati ya jiji ambapo Mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Pallongya pamoja na wateja wa Benki hiyo..Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hizo mpya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema Benki ya CRDB imeamua kuzindua huduma ya “Premier Club” pamoja na kadi maalum ya “TemboCard Visa Infinite” kwa ajili ya wateja wa kundi hilo ikiwa ni mkakati wa Benki hiyo kuboresha huduma kwa wateja ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi. “CRDB Bank Premier Club” ni kituo maalum ambacho Benki ya CRDB imekianzisha kwa ajili ya kuwahudumia wateja kundi hili maalum. Kituo hiki ambacho kipo katika jengo la “Viva Towers,” ni cha kisasa, cha kuvutia, na kimejengwa katika viwango vya kimataifa ili kuendana na hadhi ya wateja hawa” alisema Dkt. Kimei.


Dkt. Kimei alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo ya wateja maalum “Premier Banking” kutasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Benki kwa wateja huku akiamini huduma hiyo itakuwa nichachu ya kuboresha huduma kwa wateja kwa Benki hiyo kwa ujumla. “Katika kituo hiki cha Premier Club wateja wataweza kupata huduma za kipekee ambazo zinatofautisha na wateja wa makundi mengine. Mteja atakuwa akihudumiwa na mhudumu maalum ili kuhakikisha anahudumiwa kwa muda mfupi iwezekanavyo. Nina imani kubwa hii kitasaidia kuweka viwango vipya vya jinsi ya kuhudumia wateja wateja wetu” alisema Dkt. Kimei.


Akiongelea juu ya huduma zitakazotolewa katika kituo hicho cha kisasa cha “Premier Club”, Dkt. Kimei alisema wateja waliojiunga na huduma hiyo watapewa kadi maalum ijulikanayo kama “TemboCard Visa Infinite” , huku wakipewa kipaumbele katika huduma mbalimbali pamoja na kupata nafuu ya tozo na riba katika huduma watakazo zitumia. “Tunahitaji kuwafanya wateja wetu wafurahie zaidi, na ndio mana tumeamua kufanya maboresho haya. Mbali na huduma hizo mteja pia atapewa ushauri juu ya huduma mbalimbali za uwekezaji ikiwamo katika soko la hisa” alisema Dkt. Kimei.


Akielezea juu ya TemboCardVisa Infinite Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Bi. Tully Mwambapa alisema kadi hiyo ni kadi ya kifahari zaidi na imetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu kuliko kadi zote katika za kimataifa za malipo duniani. Wateja watakaopewa kadi hii ya Tembocard Visa Infinite wataweza kufurahia huduma mbalimbali za kimataifa zinazopatikana kupitia Visa, ikiwamo kupata usaidizi popote pale walipo duniani kama akipotelewa na kadi yake imepotea, ikijumuisha kutumiwa kadi nyengine pale alipo pamoja na kupatiwa fedha za zarura.


“Naomba kuzitaja baadhi tu ya huduma ambazo wateja wetu wataweza kupata kupitia kadi hii ya “TemboCardVisa Infinite”; wateja watapewa bima ya safari pamoja na familia zao endapo watafanya malipo kupitia kadi, bima na nyongeza ya waranti kwa bidhaa watakazonunua kupitia kadi zao, wateja wataweza kupata huduma katika kumbi maalum (VIP lounges) za viwanja vya ndege duniani kote, pamoja na punguzo katika maduka, hoteli, migahawa na sehemu mbalimbali za michezo duniani” alisema Bi. Tully Mwambapa.


Dkt. Kimei alisema juhudi hizo za kuanzisha huduma hiyo ya kipekee kwa wateja wa kundi hilo maalum zilianza mwaka 2008 ambapo Benki ya CRDB iliingiza sokoni huduma kwa ajili ya wateja maalum tuliyoipa jina la “Premier Banking”. Huduma ambayo ilienda sambamba na kuanzisha dawati maalum “Premier Center & Lounge” kwa ajili ya kuwahudumia wateja wa kundi hili katika matawi yetu yote nchi nzima. “Naomba niseme kuwa tokea kuanzishwa kwa huduma ya Premier Banking wateja wengi wamevutiwa na hadi kufikia Julai mwaka huu 2016 jumla ya wateja waliosajiliwa katika huduma hii imefikia wateja 8,000. Haya nimafanikio makubwa sana na ya kujivunia kwa Benki yetu” alisema Dkt. Kimei.


Akiongea katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Ndugu. Ally Laay ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza kuingiza sokoni kadi ya malipo yaani “TemboCard” ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuwapa wateja uhuru wa kupata huduma kwa muda na mahali wanapotaka. “TemboCard iliendelea kupata umaarufu zaidi pale ilipoongeza huduma ya kuweza kutumika nje ya nchi, au kupitia ATMs za mabenki mengine, baada ya kuungana na makampuni makubwa yanayotoa huduma za kadi ya Visa, MasterCard na China Union na hivyo kuunda TemboCardVisa, TemboCard MasterCard na hivi karibuni TemboCard China Union Pay” alisema Ndugu. Laay.


Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB alisema Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB ina jukumu la kuweka mazingira bora ya uzalishaji, yatakayosadia menejimenti na wafanyakazi kufikia malengo ya kibiashara huku wakiweka mahitaji ya wateja mbele zaidi. “Bodi inathamini na kutoa kipaumbele utumiaji wa teknolojia na ubunifu wa wafanyakazi wake ili kuboresha na kurahisisha huduma zake kwa wateja, na hii ndio nguzo ya pekee ambayo imeifikisha Benki yetu katika mafanikio haya makubwa amabpo leo hii tunazindua huduma hizi za “TemboCardVisa - Infinite” na kituo cha kisasa cha huduma kwa wateja wa Premier yaani “CRDB Bank Premier Club”” alisema Ndugu Ally Laay.Dkt. Tulia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kwa kizundua huduma hizo za Premier Club na TemboCardVisa Infinite, pamoja na mafanikio na ambayo benki hiyo imeyaa na kuendelea kuyapata, ambayo yana akisi sera ya serikali na adhma ya Bunge ya kutaka kujumuisha wananchi wengi zaidi katika mfumo halali wa fedha. “Mimi nikiwa kama kiongozi wa Bunge ambalo ni muhimili mkubwa wa nchi yetu, nimekuwa nikifarijika sana kwa namna ambavyo benki yetu ya CRDB imeendelea kukua na kuimarika na hivyo kuonyesha kuwa hata sisi watanzania wenyewe tunaweza Tunawapongezeni na Hongereni sana!” alisema Dkt. Tulia.


Dkt. Kimei alihitimisha hafla hiyo kwa kuwakaribisha wateja wa Benki ya CRDB na watanzania kwa ujumla kupata huduma za kipekee katika kituo hicho cha “Premier Club” kilichopo Viva Towers. “Ninajivunia kusema Benki yetu imefanikiwa tena kwa mara nyengine kuanzisha huduma yenye viwango vya kimataifa ikiwa ni mkakati wetu wa kuwahudumia wateja wetu kwa viwango vilivyo bora” alihitimisha Dkt. Kimei.


-MWISHO-

(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);