Benki ya CRDB yahitimisha kampeni ya “Tuma Pesa na Simbanking, Shinda Passo”


Dar Es Salaam Tanzania,  Desemba 10, 2015 – Benki ya CRDB leo imehitimisha kampeni yake maalumu ya utumiaji wa huduma zake ya kibenki kupitia simu ya mkononi (SimBanking) na kupitia kwa  mawakala (FahariHuduma Wakala) “Tuma Pesa na SimBanking Shinda Passo” kwa kuwa zawadia washindi wa mwisho wa kampeni hiyo zawadi mbalimbali ikiwemo zawadi za magari matatu kwa washindi wa kwanza wa miezi ya Septemba, Oktoba na Novemba. 
 
Akizungumza katika sherehe za kuhitimisha kampeni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema Benki ya CRDB mwanzoni mwa mwaka huu wa 2015 ilianzisha kampeni hiyo iliyolenga kuwasisitizia wateja wake na watanzania kwa ujumla umuhimu wa kutumia njia hizo mbadala za kibenki ili kupata huduma kwa urahisi na uharaka zaidi. Dkt. Kimei alisema kuwa kampeni hiyo ya “Tuma Pesa na SimBanking Shinda Passo” imepata mafanikio makubwa kwani idadi ya wateja wanaoutumia huduma ya Simbanking imeongezeka maradufu hadi kufikia wateja 1,800,000 huku idadi ya miamala inayofanyika kwa njia hizo mbadala ikiongezeka pia.
 

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Ndugu, Martin Mmari akikabidhi zawadi ya gari kwa Ndg. Maria Clemence Minde aliyeibuka Mshindi wa kwanza kwa mwezi Novemba


 

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Ndugu, Martin Mmari akikabidhi zawadi ya gari kwa Ndg. Hellen Solomon Achimpota aliyeibuka Mshindi wa kwanza kwa mwezi Desemba


 


Katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Ndugu, Martin Mmari alikabidhi zawadi za magari kwa washindi wa kwanza Ndg. Anthony Peter Mavunde aliyeibuka Mshindi wa kwanza kwa mwezi Septemba, Ndg. Maria Clemence Minde aliyeibuka Mshindi wa kwanza kwa mwezi Novemba na Ndg. Hellen Solomon Achimpota aliyeibuka Mshindi wa kwanza kwa mwezi Desemba. Mbali na washindi hao waliojishindia Toyota Passo kila mmoja, washindi wengine walikuwa ni Ndg. Urughu Emmanueli Ngui, Ndg. Editha Emmanuel Mully, na Ndg. William Pius Maluli waliojishindia zawadi za Solar Panel kwa kuwa washindi wa pili katika miezi hiyo. Pamoja na hao washindi watatu walizawadiwa  Samsung Tablet, ambao walikuwa ni Ndg. Saidi Rajabu Msonga, Ndg. Deogratius Liberatus Shayo na Ndg. Deogratius Paul Mushi. Hitimisho la ugawaji wa zawadi hizi zinafanya idadi ya washindi wa magari aina ya “Toyota Passo” kufikia 10 kuanzia mwenzi februari ambapo Mshindi wa kwanza wa kampeni hiyo alipatikana, Washindi watatu wa pikipiki, washindi kumi wa solar panel na  washindi zaidi ya hamsini wa  simu aina ya smartphone.
 
Dr. Kimei alisema kampeni hiyo ya “Tuma Pesa na SimBanking Shinda Passo” imesaidia sana kuleta chachu kwa watumiaji wa SimBanking na FahariHuduma kwani wengi wao waliendelea kufurahia huduma hizo huku wakijishindia zawadi mbalimbali. Dr. Kimei alifafanua kuwa wateja waliofanikiwa kuwa washindi ni wale ambao walikuwa wamefanya miamala mingi zaidi kwa kupitia njia za Simbanking au FahariHuduma katika mwezi husika, iwe ni kwenda kwenye akaunti nyingine, kwenda kwenye mitandao ya simu au kulipia Ankara.
 
Kwa mara ya kwanza Benki ya CRDB ilizindua huduma ya SimBanking mwaka 2004, ikilenga kuwapa wateja wake urahisi wa kufanya miamala ya kibenki popote walipo. Takwimu zinaonyesha kuwa huduma ya SimBanking inaongoza kwa kuwa huduma pekee ya kibenki kupitia simu ya mkononi iliyopokelewa vizuri zaidi na wateja. Urahisi, usalama na unafuu wa huduma ya SimBanking inawawezesha wateja wengi wa Benki ya CRDB kufanya miamala mbalimbali kama kutuma pesa kwenda kwenye simu za mikononi, kuhamisha pesa (kwenda akaunti nyingine za Benki ya CRDB, kwenda mitandao ya simu), kulipia karo ya shule, kulipia bili (Luku/Dawasco/Moruwasa n.k), kununua muda wa maongezi na kutoa pesa kwa Wakala wa FahariHuduma.
 
Dr. Kimei alisema pamoja na mafanikio ya Simbanking sokoni, bado watanzania wengi wako nje ya mfumo rasmi wa kibenki na hivyo Benki hiyo kwa iliadhimia kusogeza huduma zaidi kwa kupitia mfumo wa Mawakala ujulikanao kama FahariHuduma Wakala. Mawakala wa FahariHuduma hutoa huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo ikiwemo  kuweka na kutoa fedha kwenye akaunti za wateja, kutuma fedha kwa watu walio na wasio na akaunti za Benki, kupokea fedha, kupokea marejesho ya mikopo, kulipia Ankara mbalimbali, kuhamisha fedha kwenda kwenye akaunti nyingine ndani ya benki ya CRDB, kuangalia salio na kuchukua kadi za Benki ya CRDB.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Bwana Martin Mmari ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, aliwapongeza wateja wote wa Benki hiyo walioshiriki katika kampeni hiyo, huku akisisitiza kuwa bodi yake inafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha  kuwa benki ya CRDB inakuwa na njia mbadala za kutolea huduma ili kuwapa wateja wake wasaa wa kupata huduma kwa muda na mahali watakapo. “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa zile zama za kila mtu kuja kwenye tawi la benki ili kuhudumiwa zinakuwa ni historia kwani anaweza kupata huduma zetu popote alipo” alisema Ndugu Mmari.
 
 
Dkt. Kimei alimalizia kwa kutoa wateja wa Benki ya CRDB na watanzania wote kwa ujumla waendelee kutumia huduma hizo mbadala za SimBanking na FahariHuduma Wakala kwani zimekuwa na manufaa makubwa hasa katika kusogeza huduma za kibenki karibu zaidi.  
 
Ili kujiunga au kutumia huduma za Simbanking mteja wa Benki ya CRDB atahitajika kupiga namba *150*03# na kufuata maelekezo.
 
(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);