Benki ya CRDB yatoa msaada wa shilingi milioni 255 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano cha jeshi la Polisi (Call Centre).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (katikati) akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu (katikati)

Dar es Salaam Tanzania, March 22, 2016 – Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa shilingi milioni 255 kwa jeshi la polisi kwaajili ya ujenzi wa kituo cha mawasiliano cha jeshi la polisi. Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika hoteli ya Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Ernest Mangu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua kuwa ili jeshi la polisi liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, linahitaji mfumo bora wa mawasiliano kati yake na raia.”

Dkt. Kimei alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mawasiliano kati ya jeshi la polisi na rai kwani raia wamekuwa nguzo muhimu sana katika kusaidia juhudi za jeshi la polisi hasa ikizingatiwa kuwa mara nyingi wao ndio huwa mashahidi wa vitendo vya uhalifu, hivyo wakiwa na njia sahihi ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi itasaidia sana kuliwezesha jeshi la polisi kufika eneo la tukio kwa uharaka zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei

Msaada huo kwa jeshi la polisi ni sehemu ya sera maalum ya Benki ya CRDB inayolenga kusaidia jamii, ambapo Benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka, zinazo elekezwa katika shughuli za kijamii, hususani katika nyanja za elimu, afya na mazingira. Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB imeamua kuelekeza msaada huo kwa jeshi la polisi kwa kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na jeshi la polisi katika kuhakikisha kuwa kuna usalama wa raia na mali zao. “Tunatambua kuwa taifa bora ni taifa lenye usalama wa uhakika ambao huwapa wananchi amani ya uzalishaji huku wakijua kuwa familia zao ziko salama. Kinyume cha hapo, juhudi zetu za kujikwamua kutoka katika umaskini hazitafanikiwa kwani ukosefu wa usalama wa mali na jamii nzima kwa ujumla huleta hofu na sintofahamu ambazo hupunguza muda wa uzalishaji” alisema Dkt. Kimei.

Dkt alisema Benki ya CRDB ikiwa kama mdau wa maendeleo inatambua kuwa juhudi za wananchi katika kujikwamua katika umaskini hazitafanikiwa kama kutakuwa na ukosefu wa usalama wa mali na jamii nzima kwa ujumla ambapo hali hiyo huathiri na kupunguza uzalishaji. Hivyo basi kuanzishwa kwa kituo hicho cha mawasiliano ambacho kinategemea kuwa cha kisasa zaidi, kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu na hivyo kuchochea zaidi shughuli za maendeleo na hata kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Ernest Mangu aliishukuru sana Benki ya CRDB wakati akitoa hotuba yake. Alisema Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa sana wa usalama wa raia kupitia michango na misaada mbalimbali ambayo wamekuwa wakiitoa kwa jeshi hilo ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha jeshi la polisi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. IGP Mangu alisema, mbali na mahusiano hayo yaliyopo baina ya Benki ya CRDB na jeshi la polisi, pia Benki hiyo imekuwa ikitoa huduma za kibenki kwa jeshi la polisi kwa muda mrefu ambapo Benki ya CRDB imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali kwa askari polisi kupitia Chama chao cha Kuweka na Kukopa cha URA SACCOSS na huduma za kupitisha mishahara kupitia benki hiyo. Hivi karibuni pia Benki ya CRDB ilitoa msaada wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha Polisi kata ya Marangu, Mkoani Kilimanjaro uliogarimu kiasi cha shilingi milioni 125.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu

Akikabidhi mfano wa hundi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB inaamini kituo hicho kitasaidia sana kupunguza uhalifu katika jamii na hivyo kuwa chachu ya ulinzi wa amani ambayo taifa la Tanzania limekuwa likijivunia kwa kipindi kirefu. “Kituo hiki kitawezesha kulisogeza jeshi la Polisi karibu zaidi na wananchi na kushirikiana nao ili kuweza kuwalinda vizuri zaidi,” alisema Dkt. Kimei.

Akitoa shukrani kwa niaba ya jeshi la polisi Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji na utekelezaji wa mradi, Ndg. Omari Isaa aliishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo na kuahidi kuwa ujenzi wa kituo hicho utafanyika kwa kasi ili kianze kutumika mapema. “Hakuna maneno yatakayoweza kuonyesha ni jinsi gani tunaishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huu, huku nikujitolea kulikotukuka. Mbali ya kwamba ninatoa shukrani hizi kwa niaba ya jeshi la polisi lakini vilevile naomba kutoa shukrani hizi kwa niaba ya wanachi kwani msaada huu utawasaidia sana. Nilikuwa nikizungumza na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Charles Kimei nikamueleza kuwa kumbe sio kwamba tu mmekuwa wazungumzaji bali pia mmekuwa mkiishi kauli mbiu yenu ya “Benki inayomsikiliza mteja”,” alisema Ndg. Omari Issa.

Dkt. Kimei alihitimisha hafla hiyo kwa kuwasihi wananchi kutumia kituo hicho kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la polisi kwani kufanya hivyo kutasaidia sana kuboresha ulinzi na usalama katika jamii yetu. “Kipekee kabisa nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wote kwa ujumla kutumia fursa hii ya uwepo wa kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi ili kufichua maovu yanayoendelea kwenye jamii yetu. Ni ukweli usiopingika kuwa wahalifu wanaishi miongoni mwetu hivyo sisi raia ndio wenye jukumu la kwanza la kuwafichua ili sheria ichukue mkondo wake. Uboreshaji wa kituo hiki hautakuwa na maana yoyote kama bado tutaendelea kuwaficha na kuwalinda waovu”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu

Dkt. Kimei alisema wananchi wana jukumu kubwa la kuwapa ushirikiano polisi kwa kuwafichua na kuwaripoti wahalifu, kufanya hivyo, kutaweka mazingira salama. Aliwasihi wananchi kupiga namba hizo za kituo cha mawasiliano cha polisi “111” na “112” ambazo hazitatozwa gharama yoyote wakati wakutoa taarifa.

Msaada huo wa kituo cha mawasiliano cha polisi (call centre) ni moja ya misaada mingi ambayo Benki ya CRDB imetoa tokea kuanza kwa mwaka huu wa 2016, ambapo Benki ya CRDB inasherehekea miaka 20 tokea kuanzishwa kwake.

-MWISHO-

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tully Esther Mwambapa
+255 769 200 600
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu
+255 784 002020
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);