Benki ya CRDB yatoa Msaada katika Makao ya Wazee na Walemavu wasiojiweza, Bukumbi, Mwanza.

Msaada
Mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB Dr. Charles Kimei, Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mh. Magesa Mulongo pamoja na Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli

Mwanza Tanzania, Marchi 05, 2015 – Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa vifaa vya kuzalishia umeme pamoja na chakula wenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 53, ikiwa ni moja ya sehemu ya Benki hiyo katika kuisaidia jamii. Kwa kuzingatia mahitaji ya jamii inayoizunguka, Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kusaidia jamii ambayo inalenga kurudisha kiasi cha asilimia moja ya faida ya Benki hiyo kila mwaka, ili ziende katika shughuli za kijamii, hususani katika nyanja za elimu, afya na mazingira.

Akizungumza katika makabidhiano hayo ambayo yalihudhuriwa na mke wa raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa mama Janet Magufuli pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua changamoto mbalimbali wanazozipata wazee na walemavu wasiojiweza. Tunatambua kuwa taifa bora ni taifa ambalo linajali na kutambua mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa hilo. Pia tunatambua kuwa ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa wazee, walemavu na wasiojiweza katika jamii yetu wanapata matunzo stahiki.”

Akimnukuu muandishi na mtangazaji mahiri wa Kimarekani, Andy Rooney ambaye aliwahi kusema “the best classroom in the world is at the feet of an eldery person” akimaanisha kuwa mafundisho bora zaidi duniani yanapatikana kutoka kwa wazee wetu. Dkt Kimei alisema kutokana na usemi huo Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya jamii haina budi kujitoa katika kuwatunza, kuwalea na kuwaenzi wazee wetu ili kuiwezesha jamii na taifa kwa ujumla kuvuna busara zao.

Kituo cha wazee na walemavu wasiojiweza cha Bukumbi kilijengwa na kuanzishwa na serikali mwaka 1974 ili kusaidia kundi hilo maalum kwa kuwapatia matunzo na ulinzi. Toka kipindi hicho kituo hicho kimekua kikiendelea kutoa huduma kwa wazee wanaotoka sehemu mbalimbali za kanda ya ziwa. Kituo hicho kwa sasa kina jumla ya wakazi 108 ambapo kati yao wanawake ni 55 na wanaume 36 na kwa upande wa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ni 17 ikiwa wakike ni 10 na wakiume 7. Tokea kuanzishwa kwake kituo hicho kimekuwa kikiendeshwa na Serikali kupitia ustawi wa jamii lakini kutokana na changamoto mbalimbali kituo hicho kimekua kikitegemea zaidi misaada toka kwa wafadhili mbalimbali wakiwemo watu binafsi, mashirika ya misaada na taasisi za binafsi.

Msaada
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB akikabidhi sehemu ya msaada kwa Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli

Mapema mwaka huu mama Janeti Magufuli alitembelea kituoni hapo, ambapo uongozi wa kituo ulimuelezea changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikumbana nazo. Mama Magufuli alichukua changamoto hizo na kuziwasilisha kwa ungozi wa Benki ya CRDB ikiiomba Benki hiyo kuweza kusaidia kutatua changamoto zinazokikumba kituo kicho. Akiongea katika hafla hiyo ya makabidhiano ya msaada huo mke wa raisi mama Janeti Magufuli aliishukuru na kuipongeza Benki ya CRDB kwa kuonyesha moyo wa kipekee katika kuwasaidia wazee na walemavu wasiojiweza katika kituo hicho cha Bukumbi.

Akiongea wakati wa makabidhiano ya msaada huo ambao ulijumuisha vifaa vya kuzalishia umeme wa jua “Solar panel”, mchele kilo 6000, unga kilo 6000, maharage kilo 3000, mafuta ya kupikia lita 1,000, Sukari kilo 2,500, madawa mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni mbili, vitu hivyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 53 za kitanzania. Dkt. Kimei alimpongeza mama Janet Magufuli kwa kujitoa kwake katika kutafuta suluhisho la changamoto nyingi zinazowakabili wakinamama, walemavu, wazee, watoto na wasiojiweza nchini. “Ama kwa hakika huu ni moyo wa kipekee, na naomba ni seme kweli taifa la Tanzania limepata mama mlezi anayewapenda na kuwajali watoto wake” alisema Dkt. Kimei.

Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa kituo hicho Mzee Bundala ambaye pia ni Mkuu wa kituo alisema uongozi wa kituo hicho pamoja na wakazi wake wote wamefarijika sana kwa msaada huo na wanaimani utaweza kutatua changamoto zao kwa kiasi kubwa sana. “Hakuna maneno yanayoweza kuonyesha furaha yetu, tunachoweza kusema ni tunashukuru sana na tunawaombea kwa Mungu pale mlipo toa basi akawaongezee maradufu.”

Katika hotuba yake fupi mama Janeti Magufuli pia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwajali na kuwathamini wanawake na kuwa benki ya kwanza nchini kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la “Malkia Akaunti,” huduma za bima kwaajili ya kina mama “Lady Jubilee” na mikopo maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la “Mikopo ya Wafi”. Mama Magufuli alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakinamama kuweza kutumia fursa hizo zilizopo katika kukuza na kuendeleza biashara zao. “Wanawake sisi ndio nguzo ya familia hivyo fursa za akaunti za Malkia na mikopo ya WAFI ni muhimu kwa manufaa ya familia na taifa zima kwa ujumla” alisema mama Magufuli.

Dkt. Kimei alihitimisha hotuba hiyo fupi kwa kumuhakikishia mama Magufuli kuwa Benki hiyo ipo pamoja na wakina mama huku akimuomba kuwa balozi wa fursa hizo zinazopatikana ndani ya Benki ya CRDB kwa kuwafikishia ujumbe wa bidhaa na huduma hizo wakina mama pindi atapopata fursa ya kukutana nao.

-MWISHO-

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tully Esther Mwambapa
+255 769 200 600
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu
+255 784 002020
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);