PRESS RELEASE: Benki ya CRDB yazindua maadhimisho ya sherehe za miaka 20 toka kuanzishwa kwake,

Dar Es Salaam Tanzania, Februari 17, 2016– Benki ya CRDB imezindua sherehe za maadhimisho ya miaka ishirini ya benki hiyo katika hoteli ya Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Mwaka huu Benki ya CRDB inaadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwake hivyo basi tumeona ni vyema tukasherehekea mafanikio tuliyoyapata ndani ya kipindi hiki pamoja na wateja wetu. Sisi sote tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa benki ya CRDB hasa katika rasilimali, amana, mtandao wa matawi, mikopo na uchangiaji mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.”

Akielezea historia ya Benki ya CRDB, Dkt. Kimei alisema benki hiyo ilianzishwa tarehe 1 mwezi Julai mwaka 1996 kufuatia kutofanya vizuri kwa iliyokuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini iliyojulikana kama Cooperative Rural Development Bank. Dkt. Kimei alisema kuwa benki ilikabiliwa na matatizo mbalimbali katika uendeshaji wakati wa kuanzishwa kwake ikiwamo mfumo duni wa Tehama ambao ulileta changamoto kubwa hasa katika utunzaji wa mahesabu. Kutokana na mwanzo kuwa mgumu benki hiyo ilipata hasara ya jumla ya shilingi bilioni 1.8 mwaka uliofuatia yaani mwaka 1997. Baada ya mwaka huo benki ilijipanga vizuri na imekuwa ikiendelea kupata faida mwaka hadi mwaka na kukua na kustawi hadi kufikia kuwa benki inayoongoza Tanzania.

Dkt. Kimei alisema hadi kufikia Desemba 2015 Benki ya CRDB imekua maradufu kutoka matawi 19 yaliyokuwa na jumla ya wafanyakazi 400 wakati ilipoanzishwa hadi kufikia matawi 198 na jumla ya wafanyakazi 2,682, huku idadi ya wateja ikiongezeka hadi kufikia 1,800,000 kutoka 120,000 ambao benki ilianza nao. “Ama hakika tumepiga hatua kubwa sana ukilinganisha na pale tulipoanzia kwani pamoja na mafanikio hayo, vilevile amana za benki zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 40 hadi shilingi trilioni 4.2, mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 2 hadi kufikia shilingi trilioni 3.3, wakati jumla ya Rasilimali imeongezeka kutoka shilingi bilioni 54 hadi kufikia shilingi trilioni 5.4,” alisema.

Benki ya CRDB imekuwa ikisifika kwa kuongoza kwa ubunifu wa bidhaa na huduma mbambali ikilenga kuwahudumia wateja wake vizuri zaidi na kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla. Ikiienenda sambamba na kauli mbiu yake ambayo imejielekeza katika kuwajali wateja “Benki ninayomsikiliza mteja,” Benki ya CRDB ndio iliyokuwa benki ya kwanza Tanzania kuingiza sokoni Mfumo wa Malipo kwa kutumia Kadi (TemboCard), Mashine maalumu za kuwekea fedha (ATMs), Huduma za benki kupitia simu ya mkononi (SimBanking), Matawi yanayo tembea, Vifaa maalumu vya kulipia manunuzi (PoS), Huduma za kibenki kupitia mtandao (Internet Banking), Kituo cha Huduma kwa Wateja, huduma za biashara kupitia mtandao wa intanenti, Huduma kupitia madawati ya kimataifa ya China na Indian Desk, na huduma za kibenki kupitia mawakala (FahariHuduma Wakala) ambao sasa wamefikisha mawakala 1,769 nchi nzima.

read more

Dkt. Kimei alisema kuwa katika ukuaji huu wa Benki ya CRDB, pia wamefanikiwa kuanzisha kampuni mbili tanzu za “CRDB Bank Microfinance” inayojihusisha na biashara na mikopo kwa wakulima na wafanyabishara wadogo wadogo na CRDB Bank-Burundi ambayo imefunguliwa nchini Burundi ili kujenga daraja la kibiashara kati ya nchi hizi mbili. Kampuni hizo zimeongeza chachu kubwa katika ukuaji wa biashara ya benki hiyo pamoja na kuiletea umaarufu katika nchi za kanda ya afrika ya mashariki na kati.

Akizungumza kuhusu mchango wa benki hiyo katika maendeleo na ustawi wa jamii Dkt. Kimei alisema, “Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kuchangia kwenye mahitaji ya jamii ambapo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida yake ili itumike kusaidia katika maeneo ya elimu, afya na mazingira. Kwa mfano mwaka 2015 benki yetu ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 katika kusaidia jamii inayoizunguka.”

Akielezea siri ya mafanikio hayo yaliyopatikana katika kipindi hicho, Dkt. Kimei alisema siri kubwa ni uwepo wa wafanyakazi wazuri, wenye kutii masharti yanayoendana na utamaduni wa biashara waliojiwekea, pamoja na kuwa wabunifu. Pia aliwashukuru wanahisa wa Benki hiyo kwa ushirikiano wanaotoa kwa uongozi wa Benki ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ambayo Benki imejiwekea. Katika mwendelezo wa shukrani zake Dkt. Kimei aliishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kiabashara ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa ustawi wa taasisi nyingi za kifedha nchini.

Dkt. Kimei alihitimisha kwa kuwashukuru wateja na wadau wengine wa Benki ya CRDB ambao kwa namna moja au nyingine wamechaingia kufanikisha mafanikio ya Benki hiyo huku akiwasihi waendelee kutumia bidhaa na huduma za Benki hiyo kwani Benki ya CRDB imejipanga vizuri katika kuboresha huduma na maisha ya wateja wake. Wadau mbalimbali waliohudhria katika uzinduzi wa maadhimisho ya sherehe hizo wamesema mafanikio haya makubwa iliyoipata Benki ya CRDB yanatokana uongozi bora wa wazawa na ubunifu wake kwenye bidhaa na huduma wanazotoa ambazo zimepelekea benki hiyo kutambulika, kuthaminiwa na kuwa chaguo nambari moja kwa wateja.

Benki ya CRDB imekuwa ikipata tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2004 benki hiyo ilipata tuzo ya ubora wa huduma ya “Euro Money” iliyotolewa na jumuiya ya mabenki barani ulaya. Benki pia imeweza kujitwalia tuzo ya umahili wa chapa yaani “Superbrand” kwa miaka mitano mfululizo toka mwaka 2010 na tuzo wa “Muajiri bora wa mwaka” inayotolewa na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE) kwa zaidi ya miaka sita mfululizo.

-MWISHO-

(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);