HOTUBA YA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA CRDB DKT. CHARLES KIMEI KATIKA UZINDUZI WA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA BENKI YA CRDB ZILIZOFANYIKA KATIKA HOTELI YA RAMADA ENCORE JIJINI DAR ES SALAAM, JUMATANO TAREHE 17/02/2016.

Wapendwa Wageni Wetu Rasmi wa Siku ya Leo, ambao ndio Ninyi Waandishi wa Habari

Ndugu Manaibu Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya CRDB

Ndugu Wakurugenzi wa Makao Makuu pamoja na Matawi ya Benki ya CRDB

Ndugu Mameneja na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB

Habarini za asubuhi,

Wapendwa Wageni Rasmi

Kama wengi wenu mtakavyokumbuka, Benki yetu ya CRDB ilianzishwa mwezi Juni mwaka 1996 kufuatia marekebisho makubwa ya kiutawala, kimuundo na kifedha yaliyofanywa kuanzia mwaka 1991 na kuiweka Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB) kwenye hali ya kuweza kubinafsishwa. Benki hii ilianzishwa ikiwa na Mizania ndogo iliyojumuisha Amana zenye thamani za TZS 40 bilioni na Raslimali za TZS 54 bilioni, ikiwa imeshikilia asilimia 5 tu ya jumla la rasilimali za mabenki yaliyokuwepo nchini.

Aidha Benki mpya ya CRDB ilikuwa na matawi 19 tu na mfumo duni wa Tehama, ambapo kila tawi lilikuwalinajitegemea kiuendeshaji likiwa na mfumo wake wakutunza mahesabu yaliyotokana na mfumo duni (uncomputerized system) wa kutolea huduma kwa wateja. Kutokana na mwanzo huu mgumu, katika mwaka wa pili (1997) Benki ilipata hasara ya jumla ya shilingi bilioni 1.8. Baada ya mwaka huo Benki imeendelea kupata faida mwaka hadi mwaka na kukua na kustawi kama mtoto anayepata Jazia Lishe.

Ndugu wageni waalikwa,

Toka ilipoanzishwa, uendeshaji wa Benki ya CRDB uliongozwa na azma ya kutumia ubunifu na Teknolojia ili kuwahudumia wateja vizuri na kujijengea uwezo wa kuunda bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja kwa kasi inayostahili. Lengo la misingi hii lilikuwa ni kujenga Benki imara inayoongoza Tanzania kwa kuwafikishia wananchi wengi huduma muhimu za kifedha.

Hotuba
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei akiongea na waandishi katika ufunguzi wa maadhimishi ya Miaka 20 ya Benki ya CRDB.
Hotuba
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na huduma kwa wateja wa Benki ya CRDB, Bi. Tully Mwambapa akiongea na waandishi katika ufunguzi wa maadhimishi ya Miaka 20 ya Benki ya CRDB
Hotuba
Naibu mkurugenzi mtendaji Huduma Shirikishi wa Benki ya CRDB, Bi. esther Kitoka akiwa na baadhi ya wakurugenzi wa Benki ya CRDB
Hotuba
Baadhi ya wakurugenzi wa Matawi ya Benki ya CRDB
Hotuba
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei, Naibu Mkurugenzi (Huduma Shirikishi) Bi. Esther kitoka pamoja na Baadhi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB
Hotuba
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei katikati akiwa na manaibu wakurugenzi watendaji wa Benki ya CRDB, Mr. Saugata Bandyopadhyay kushoto na Bi. Esther Kitoka
Hotuba
Baadhi ya Wakurugenzi na Mameneja wa matawi ya CRDB
Hotuba
Baadhi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB
Hotuba
Baadhi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB

Ndugu waandishi wa habari, Katika kipindi cha miaka ishirini, sisi sote tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa benki ya CRDB hasa katika rasilimali, amana, mtandao wa matawi, mikopo na uchangiaji mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

Ndugu wageni waalikwa, Hadi kufikia Desemba 2015 Benki ya CRDB inajivunia mafanikio yafuatayo ya takriban miaka ishirini ya kutekeleza dira yake na Mipango Mikakati iliyoshabihiana na dira hiyo: Mtandao wetu wa matawi ya kawaida na yale yanayotembea ulikuwa umepanuka kutoka matawi 19 mwaka 1996 hadi kufikia matawi 198, ikiwa ni ongezeko mara 10. Lakini licha ya matawi ya kawaida, mtandao wetu ulikuwa unajumuisha vituo mbadala vya kutolea huduma kwa wateja kama ifuatavyo:

1. ATMs 461,
2. Fahari Huduma Wakala 1769,
3. Vituo vya kutoa huduma kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 40,
4. SACCOs zilizoingia ubia na Kampuni Tanzu yetu ya CRDB Microfinance Services, 482, na
• Vifaa vya kutolea huduma kwenye vituo mbalimbali vya biashara kama vile mahoteli, supermarkets, mahospitali n.k 989.
• Idadi ya wateja iliongezeka kutoka 120,000 hadi kufikia wateja 1,800,000 (milioni moja na laki nane)
• Amana za Benki ziliongezeka kutoka TZS bilioni 40 hadi shilingi trilioni 4.2
• Mikopo iliongezeka kutoka TZS bilioni 2 mwaka 1996 hadi kufikia shilingi trilioni 3.3
• Jumla ya Raslimali (total assets) ziliongezeka kutoka TZS bilioni 54 hadi kufikia TZS trilioni 5.3
• Jumla ya wafanyakazi iliongezeka kutoka 400 mwaka 1996 na kufikia 2,682.
• Tulikuwa wa kwanza kuunganisha matawi yetu ili kufanya kazi kama tawi moja na hivyo kuwezesha uhamishaji wa fedha kutoka tawi moja kwenda jingine papo kwa papo tangu mwaka 1999.
• Tulikuwa wa kwanza kuanzisha mfumo wa kutoa huduma kwa wateja wetu kwa kutumia kadi za ATM mwaka 2002: Hadi leo hii tuna kadi za Visa na Mastercard zinazofikia 1,400,000; na tuko mbioni kuanza kutoa card za China Union Pay ambazo tayari zinakubalika kwenye ATM zetu.
• Tulikuwa wa kwanza kubuni bidhaa inayokidhi mahitaji ya watoto (Junior Jumbo Account) na wanafunzi (Scholar Account) ambazo leo hii mabenki yote yameiga—na bahati mbaya wengine wakachua majina hayohayo bila kujali sheria zinazolinda chapa.
• Tumekuwa wa kwanza kuingiza bidhaa mahsusi ya uwekezaji inayolenga Wanawake—Malkia Account.
• Tumekuwa wa kwanza kuona fursa katika kuwapelekea huduma za kibenki kwa watanzania wanaoishi nchi za nje: Akaunti yenye chapa ya Tanzanite.
• Na mengine mengi tumefanya!

Ndugu wageni waalikwa, Tukiangalia nyuma tulikotoka, tunapata kila sababu ya kuwashukuru sana wateja wetu kwani mwaka 1996 wakati benki hii inaanzishwa, ilikuwa ikitoa huduma chache sana kama ifuatavyo:
1. Huduma za kufungua akaunti mbalimbali
2. Huduma za mikopo
3. Huduma za kutoa, kuweka na kubadili fedha

Ndugu wageni waalikwa,
Kama nilivyoorodhesha hapo juu, Benki yetu ina mengi ya kujivunia, lakini nisisitize uwepo wa Wafanyakazi wazuri, wenye kutii masharti yanayoendana na utamaduni wa biashara tuliojiwekea (Corporate Culture and Values), na hivyo kuwa wabunifu sana ndio siri ya mafanikio yetu. Naomba nirudie kutaja baadhi ya huduma ambazo ni bunifu na kila ninapokuwa na muda wangu wa pekee ninajipiga kifua na kusema, ama kweli hapa tumefanya. Huduma hizi ni kama zifuatazo:

• Huduma kupitia simu za mikononi yaani “Simbanking”
• Huduma kupitia mtandao wa yaani “Internet Banking”
• Huduma kupitia matawi yanayotembea yaani “mobile branches”
• Huduma kupitia mawakala wa FahariHuduma
• Huduma kupitia ATM zinazofikia 461
• Huduma kupitia madawati ya kimataifa ya China na Indian Desk, na • Huduma kupitia kadi za kimataifa za TemboCardVisa, TemboCardMasterCard na TemboCard China Union Pay.

Ndugu waandishi wa habari,
Katika ukuaji huu Benki ya CRDB imepata watoto wawili wenye afya nzuri ambao wanajitegemea na kutoa huduma kwa wateja ndani na nje ya nchi. Watoto hawa ni Kampuni tanzu ya “CRDB Bank Microfinance” inayojihusisha na biashara na mikopo kwa wakulima na wafanyabishara wadogo na kampuni tanzu ya CRDB Bank-Burundi ambayo imefunguliwa nchini Burundi ili kujenga daraja la kibiashara kati ya nchi hizi mbili.

Ndugu wageni waalikwa,
Benki ya CRDB kwa uhakika imeacha alama katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita. Sisi sote tunajua kwamba Benki ya CRDB inajulikana sana ndani na nje ya nchi kama kielelezo cha hadithi ya mafanikio(success story) ya sera ya ubinafsishaji nchini. Uongozi bora wa wazawa na ubunifu kwenye bidhaa na huduma zinaifanya Benki ya CRDB kutambulika, kuthaminiwa na kuzawadiwa tuzo mbalimbali na vyombo na taasisi za kitaifa na kimataifa.

Katika kipindi hiki Benki ya CRDB imekuwa ikipata tuzo mbalimbali mfano ni mwaka 2004 Benki ilipata tuzo ya ubora wa huduma ya “Euro Money” iliyotolewa na jumuiya ya mabenki barani ulaya. Benki pia imeweza kujitwalia tuzo ya umahili wa chapa yaani “Superbrand” kwa miaka mitano mfululizo toka mwaka 2010 na tuzo wa “Muajiri bora wa mwaka ” inayotolewa na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE) kwa zaidi ya miaka 6 mfululizo.

Ndugu wageni waalikwa,
Jambo moja kubwa la kujivunia ni kwamba Kampuni zetu tanzu, ikwemo CRDB Bank Burundi, zinafanya faida nzuri. Juu ya hilo Benki imeendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya taifa letu kama ifuatavyo:

1. Kinara wa ulipaji kodi
Benki ya CRDB imeendelea kuwa kinara wa ulipaji kodi (Corporate tax) ambapo kwa mwaka 2015 tumelipa TZS bilioni 42. Kama tukijumuisha kodi nyingine zilizolipwa na Benki yetu, kama vile Excise Duty kwenye tozo mbalimbali na kodi kwa mishahara ya wafanyakazi basi Benki ililipa jumla ya TZS bilioni 70. Tumekuwa kinara wa ulipaji kodi kati ya mabenki na makampuni mengine nchini.

2. Nafasi za ajira na mafunzo ya kazi,
Mpaka kufikia mwezi Disemba 2015, Benki ya CRDB imeshatoa ajira za kudumu zaidi ya 2682 ambapo asilimia 99.99% ni ajira kwa wazawa. Benki pia ina utaratibu maalum wa kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kupata mafunzo ya kazi yaani “field attachment” na “internship,” ambapo kila mwaka zaidi ya wanafunzi 500 hujiunga na Benki kwa vipindi vya kati ya miezi mitatu mpaka mwaka mmoja ili kujifunza.

3. Mikopo kwa biashara na kilimo na wajasiliamari
Benki ya CRDB inajivunia kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya taifa kupitia utoaji wa mikopo mbalimbali ya kilimo, biashara, ujenzi na elimu. Zaidi ya asilimia 30% ya mikopo yote inayotolewa huingia katika sekta ya kilimo. Licha ya sekta hii kukumbwa na misukosuko ya biashara katika soko la dunia mikopo kwenda kwenye sekta ya kilimo imekua kutoka shilingi bilioni 229 mwaka 2008 hadi kufika shilingi bilioni 632 mwaka 2015.

4. Misaada kwa jamii
Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kuchangia kwenye mahitaji ya jamii ambapo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida yake ili itumike kusaidia maeneo ya elimu, afya na mazingira. Kwa mfano, mwaka 2015, Benki ilitumia zaidi ya TZS bilioni 1.2.

Ndugu wageni waalikwa, waandishi wa habari
Benki ya CRDB imejipanga kusheherekea miaka yake 20 kupitia kampeni maalum iitwayo “Miaka 20 ya Kukua Pamoja na Kuboresha Maisha” ambayo itaanza rasmi leo na kufikia kilele chake mwezi Juni mwaka huu.

Kampeni hii ina lengo la kutambua, kushukuru na kuthamini mchango wa wateja na wadau wetu katika kutufikisha hapa leo. Kampeni hii itahusisha mambo mbalimbali ikiwemo:
• Misaada kwa jamii hasa kwenye eneo la elimu, ambako Benki inaamini ndio msingi wa kweli wa maendeleo ya Taifa letu.
• Kutambua wateja walio nasi kwa muda mrefu
• Kutambua na kupongeza wafanyakazi
• Promosheni ya bidhaa na akaunti ambazo zitaambatana na zawadi nono kwa wateja wetu, na • Kuwatambua Wanahisa wetu waanzilishi.

Ndugu wageni waalikwa,
Nimalize kwa kutoa shukrani zangu binafsi, shukrani za Bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa wateja wetu na wadau wengine wote ambao kwa namna moja au nyingine wamechaingia kuifikisha Benki ya CRDB hapa tuliko leo. Nawahakikishieni wateja wetu kuwa miaka hii 20 ni mwanzo tu wa miaka mingine 20 ya mafanikio na ushirikiano zaidi.

ASANTENI SANA

(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);