Benki ya CRDB yatoa msaada wa shilingi milioni 255 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano cha jeshi la Polisi (Call Centre).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (katikati) akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu (katikati)

Dar es Salaam Tanzania, March 22, 2016 – Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa shilingi milioni 255 kwa jeshi la polisi kwaajili ya ujenzi wa kituo cha mawasiliano cha jeshi la polisi. Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika hoteli ya Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Ernest Mangu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua kuwa ili jeshi la polisi liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, linahitaji mfumo bora wa mawasiliano kati yake na raia.”

Dkt. Kimei alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mawasiliano kati ya jeshi la polisi na rai kwani raia wamekuwa nguzo muhimu sana katika kusaidia juhudi za jeshi la polisi hasa ikizingatiwa kuwa mara nyingi wao ndio huwa mashahidi wa vitendo vya uhalifu, hivyo wakiwa na njia sahihi ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi itasaidia sana kuliwezesha jeshi la polisi kufika eneo la tukio kwa uharaka zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei

Msaada huo kwa jeshi la polisi ni sehemu ya sera maalum ya Benki ya CRDB inayolenga kusaidia jamii, ambapo Benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka, zinazo elekezwa katika shughuli za kijamii, hususani katika nyanja za elimu, afya na mazingira. Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB imeamua kuelekeza msaada huo kwa jeshi la polisi kwa kutambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na jeshi la polisi katika kuhakikisha kuwa kuna usalama wa raia na mali zao. “Tunatambua kuwa taifa bora ni taifa lenye usalama wa uhakika ambao huwapa wananchi amani ya uzalishaji huku wakijua kuwa familia zao ziko salama. Kinyume cha hapo, juhudi zetu za kujikwamua kutoka katika umaskini hazitafanikiwa kwani ukosefu wa usalama wa mali na jamii nzima kwa ujumla huleta hofu na sintofahamu ambazo hupunguza muda wa uzalishaji” alisema Dkt. Kimei.

Dkt alisema Benki ya CRDB ikiwa kama mdau wa maendeleo inatambua kuwa juhudi za wananchi katika kujikwamua katika umaskini hazitafanikiwa kama kutakuwa na ukosefu wa usalama wa mali na jamii nzima kwa ujumla ambapo hali hiyo huathiri na kupunguza uzalishaji. Hivyo basi kuanzishwa kwa kituo hicho cha mawasiliano ambacho kinategemea kuwa cha kisasa zaidi, kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu na hivyo kuchochea zaidi shughuli za maendeleo na hata kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Ernest Mangu aliishukuru sana Benki ya CRDB wakati akitoa hotuba yake. Alisema Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa sana wa usalama wa raia kupitia michango na misaada mbalimbali ambayo wamekuwa wakiitoa kwa jeshi hilo ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha jeshi la polisi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. IGP Mangu alisema, mbali na mahusiano hayo yaliyopo baina ya Benki ya CRDB na jeshi la polisi, pia Benki hiyo imekuwa ikitoa huduma za kibenki kwa jeshi la polisi kwa muda mrefu ambapo Benki ya CRDB imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali kwa askari polisi kupitia Chama chao cha Kuweka na Kukopa cha URA SACCOSS na huduma za kupitisha mishahara kupitia benki hiyo. Hivi karibuni pia Benki ya CRDB ilitoa msaada wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha Polisi kata ya Marangu, Mkoani Kilimanjaro uliogarimu kiasi cha shilingi milioni 125.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu

Akikabidhi mfano wa hundi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB inaamini kituo hicho kitasaidia sana kupunguza uhalifu katika jamii na hivyo kuwa chachu ya ulinzi wa amani ambayo taifa la Tanzania limekuwa likijivunia kwa kipindi kirefu. “Kituo hiki kitawezesha kulisogeza jeshi la Polisi karibu zaidi na wananchi na kushirikiana nao ili kuweza kuwalinda vizuri zaidi,” alisema Dkt. Kimei.

Akitoa shukrani kwa niaba ya jeshi la polisi Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji na utekelezaji wa mradi, Ndg. Omari Isaa aliishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo na kuahidi kuwa ujenzi wa kituo hicho utafanyika kwa kasi ili kianze kutumika mapema. “Hakuna maneno yatakayoweza kuonyesha ni jinsi gani tunaishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huu, huku nikujitolea kulikotukuka. Mbali ya kwamba ninatoa shukrani hizi kwa niaba ya jeshi la polisi lakini vilevile naomba kutoa shukrani hizi kwa niaba ya wanachi kwani msaada huu utawasaidia sana. Nilikuwa nikizungumza na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Charles Kimei nikamueleza kuwa kumbe sio kwamba tu mmekuwa wazungumzaji bali pia mmekuwa mkiishi kauli mbiu yenu ya “Benki inayomsikiliza mteja”,” alisema Ndg. Omari Issa.

Dkt. Kimei alihitimisha hafla hiyo kwa kuwasihi wananchi kutumia kituo hicho kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la polisi kwani kufanya hivyo kutasaidia sana kuboresha ulinzi na usalama katika jamii yetu. “Kipekee kabisa nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wote kwa ujumla kutumia fursa hii ya uwepo wa kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi ili kufichua maovu yanayoendelea kwenye jamii yetu. Ni ukweli usiopingika kuwa wahalifu wanaishi miongoni mwetu hivyo sisi raia ndio wenye jukumu la kwanza la kuwafichua ili sheria ichukue mkondo wake. Uboreshaji wa kituo hiki hautakuwa na maana yoyote kama bado tutaendelea kuwaficha na kuwalinda waovu”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Ernest Mangu

Dkt. Kimei alisema wananchi wana jukumu kubwa la kuwapa ushirikiano polisi kwa kuwafichua na kuwaripoti wahalifu, kufanya hivyo, kutaweka mazingira salama. Aliwasihi wananchi kupiga namba hizo za kituo cha mawasiliano cha polisi “111” na “112” ambazo hazitatozwa gharama yoyote wakati wakutoa taarifa.

Msaada huo wa kituo cha mawasiliano cha polisi (call centre) ni moja ya misaada mingi ambayo Benki ya CRDB imetoa tokea kuanza kwa mwaka huu wa 2016, ambapo Benki ya CRDB inasherehekea miaka 20 tokea kuanzishwa kwake.

-MWISHO-

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tully Esther Mwambapa
+255 769 200 600
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu
+255 784 002020
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

CRDB Bank yatoa Mkopo wa Shilingi Bilioni 19.7 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ili kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi wa Maendeleo wa jiji la Dar es Salaam

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Abdalah Chaurembo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei na Katibu wa Kampuni, Bw. John Rugambo wakitia saini mkataba wa makubaliano

Dar es Salaam Tanzania, March 9, 2016 – Benki ya CRDB imetoa mkopo wa shilingi za kitanzania bilioni 19.7 kwa Manispaa ya Temeke iliyopo jijini Dar es Salaaam, ili kulipa fidia na kukamilisha taratibu za utekelezaji wa mpango mkubwa wa maendeleo wa jiji yaani “Dar es Salaam Metropolitan Developmenmt Project (DMDP)”

Manispaa ya Temeke ikiwa ni mojawapo ya manispaa tatu za jiji la Dar es Salaam, inahitaji mkopo huo ili kufanikisha fidia za utekelezaji wa zoezi hili ambao itahususisha ubomoaji wa baadhi ya makazi ili kupisha ujenzi wa miundombinu. Mradi maendeleo wa jiji la Dar es Salaam utahusisha kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilomota 81.63, ununuzi wa magari ya taka, ujenzi wa masoko nane ya kisasa, ujenzi wa vituo vya mabasi, upimaji wa viwanja eneo la kijichi, ujenzi wa mifereji na ujenzi wa dampo la kisasa katika eneo la Kisarawe.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Mkopo huo iliyofanyika katika hoteli Serana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt.Charles Kimei alisema kuwa Benki imekubali kutoa mkopo kwa Manispaa ya Temeke ili kusaidia kulipa fidia kwa watakaohamishwa ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo utakaokuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na taifa zima kwa ujumla” ‘’Jumla ya fedha za mkopo ni shilingi bilioni 19.7 ambapo shilingi bilioni 5 zitalipwa fidia ya upanuzi wa barabara, shilingi bilioni 12.6 zitalipwa kama fidia ya mradi wa maboresho ya makazi yasiyopimwa na shilingi bilioni 2.5 ni kwa ajili ya maeneo yatakayopisha ujenzi wa mifereji” alisema.

Lengo letu siku zote limekuwa ni kutoa huduma za kifedha zenye kuleta maendeleo ya ukweli ya kiuchumi kwa watanzania wote, iwe ni kwa mtu mmoja mmoja, kikundi au taasisi. Tunaamini kuwa mkopo huu wa riba nafuu utaisidia manispaa ya Temeke kufikia malengo yake ya maendelo bila kuathiri shughuli zake za kila siku za uendeshaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB akimkabidhi mfano wa hundi Mkuu wa Wilaya ya Temeke, mama Sophia Mjema

Tunafurahi kuendelea kuwa wadau wakubwa wa maendeleo nchini kwa kutoa mikopo ya maendeleo kwa serikali zetu za mitaa na hivyo kuwafikia watanzania wengi zaidi. Benki ya CRDB inakaribisha halmashauri zote nchini kuchukua mikopo ya maendeleo kwani mpaka sasa benki imeshakopesha halmashauri kadhaa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama ifuatavyo;

• Halmashauri ya jijji la Mwanza: shilingi 1.2 bilioni kwa ujenzi wa maabara za sekondari
• Halmashauri ya Mji wa Magu: Shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa maabara
• Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni : Shilingi bilioni 7.7 kwa ujenzi wa mitaro eneo la Boko na shilingi 1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sekondari
• Halmashauri ya Jiji la Mbeya: Shilingi 17 bilioni kwa ajili ya Ujenzi wa soko la kimataifa eneo la Mwanjelwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi.Sofia Mjema alisema kuwa serikali inathamini sana ushirikiano kati yake na sekta binafsi hususan benki ya CRDB katika kuleta maendeleo na kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii. “Kipee niwapongeze viongozi wa Benki ya CRDB na wa Manispaa ya Temeke kwa kuwa wabunifu na kufikia makubaliano haya. Ni wazi kuwa bila mkopo huu Manispaa ingebidi kutumia mapato yake yote ili kulipia fidia kabla ya kuanza mradi huu mkubwa, jambo hili lingeathiri sana shughuli za kila siku za kiuendeshaji pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii ya Temeke” alisema “Rai yangu kwa viongozi wa manispaa ni kuhakikisha kuwa mkopo huu unatumiwa kwa makusudio yake ili kuleta tija” alimalizia.

MWISHO

For More information, please contact:

Tully Mwambapa +255222112113
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu 0768002020
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Benki ya CRDB Yaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Kipekee.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Joel Laurent, Naibu waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mama Stella Manyanya, Naibu Mkurugenzi wa Benki ya CRDB-Huduma Shirikishi, Esther Kitoka na Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Huduma za Wateja Binais(Retail Banking), Nellie Ndosa, wakikabidhi mfano wa Hundi kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Dar Es Salaam Tanzania, Marchi 7, 2016– Benki ya CRDB imeungana na taasisi nyingine duniani kusherehekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Ramada Encore katika ya Jiji la Dar es Salaam. Akiongea katika hafla ya maadhimisho hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema “Lengo kuu la hafla hii ni kuwafungua macho wakinamama kuhusu fursa nyingi za kifedha zinazopatikana katika Benki yetu ya CRDB, fursa ambazo wakina mama wakizichangamkia zitawawezesha kuboresha na kubadili kabisa maisha yao, hivyo kujikwamua kiuchumi.

Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani kwa mwaka huu ni ahadi ya usawa ambayo inalenga kuihamasisha jamii katika kuwapa vipau mbele akinamama hasa katika mambo ya msingi kama ajira, elimu na uchumi. Dkt. Kimei alisema mbali na kauli mbiu hiyo Benki ya CRDB imetengeneza kauli mbiu maalamu ya “Jiwezeshe” ambayo imelenga kuwaelimisha wanawake namna ambavyo wanaweza kutumia fursa zinazotolewa na Benki hiyo katika kufanikisha ndoto zao. Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB inatambua kuwa changamoto kubwa inayowakabili wakinamama wajasiliamari wa Tanzania, hususani wafanyabishara na wajasiliamali, ni ukosefu wa mitaji. Ili kutatua hilo Benki hiyo imeweza kuingiza sokoni bidhaa na huduma maalumu kwaajili ya kina mama ikilenga kutatua changamoto hizo. Dkt. Kimei alisema bidhaa hizo ambazo Benki imekuwa ikijivunia ni pamoja na Akaunti ya Malikia, Mikopo ya WAFI pamoja na huduma za bima za Lady Jubilee.

Akielezea kuhusiana na bidhaa na huduma hizo Dkt. Kimei alisema, “Akaunti ya Malkia ni akaunti au mfumo maalum wa ulioanzishwa na Benki hiyo ili kuwawezesha wakinamama kujiwekea akiba ili kutimiza malengo waliyojiwekea, kama vile kujiendeleza kielimu, kupeleka watoto shule, kujijengea nyumba na kuongeza mitaji ya biashara. Mpango huu unampa mwanamke fursa ya kujiwekea kiasi fulani cha fedha kila mwezi bila kuathiri matumizi yake muhimu na pia kujipatia faida inayotokana na riba ya kila mwezi.” Dkt Kimei aliwapongeza wakina mama ambao tayari wameshafungua akaunti ya Malkia ambao mpaka mwishoni mwa mpaka sasa wamefikia 7,694, huku akiwataka wakinamama wengine nao waweze kuchangamia fursa hiyo kwani vigezo vya kufungua akaunti hiyo ni nafuu kabisa. “Kuna faida kubwa sana kwa wakina mama wanapokuwa na akaunti ya Malkia kwani njia rahisi ya kufikia malengo binafsi, ina riba nzuri kwa amana, hakuna makato ya kila mwezi na mama anaweza kupata mkopo wa dharura wa hadi asilimia 90 ya amana zake.” Alisema Dkt. Kimei.

Kuhusu huduma za mikopo Dkt. Kimei alisema Benki ya CRDB pia imebuni mikopo maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kama WAFI yaani “Women Access to Finance Initiatives’, Mikopo ambayo inalenga kuwakomboa wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fedha za uendeshaji wa biashara na uwekezaji wa kupanua biashara zao. Dkt. Kimei alisema mikopo ya “WAFI” imepokelewa vizuri sana sokoni kwani zaidi ya wakinamama 500 wameshapewa mikopo hiyo na tayari Benki ya CRDB imeshakopesha zaidi ya kiasi cha Shilingi bilioni 24.7 zimeshakopeshwa. Dkt. Kimei aliwasihi wakina mama kutumia huduma hiyo ya mikopo ya WAFI katika kukuza na kuendeleza bidhaa zao, hasa ukizingatia kuwa mikopo hii imeletwa kwaajili ya kuwasidia wakina mama pekee. Dkt. Kimei alisema vilevile Benki ya CRDB kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Jubilee imeingiza sokoni bidhaa ya bima ya magari (Motor insurance), mahususi kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kama “Lady Jubilee”. Huduma ambayo hutolewa kwa magari binafsi tu ya kina mama.

Katika hafla hiyo Benki ya CRDB ilikabidhi hundi ya kiasi cha shilingi milioni 20 kwa Taasisi ya Elimu nchini (Tanzania Education Authority), kwaajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari. Akiwasilisha msaada huo kwa muwakilishi wa TEA, Dkt. Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua changamoto wanazozipata wanafunzi wa kike mashuleni mojawapo ikiwa ni ukosefu wa mabweni katika shule wanazosoma na hivyo kuwaladhimu wengine kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi nyumbani au bweni moja kutumia na idadi kubwa ya wanafunzi ambayo ni hatarishi. Hivyo basi Benki kupitia sera yake ya kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii imeamua kutoa msaada huu kwasasa na tutakuwa tunafanya hivi mara kwa mara tukisaidiana na wadau wengine wa elimu ili kuweza kutatua tatizo hili.” Benki ya CRDB imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwamo kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, vyoo, vitabu, vifaa mbalimbali vya kufundishia pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi ikiwa na lengo la kuboresha na kukuza kiwango cha elimu nchini.

Prof. Ndalichako aliipongeza Benki ya CRDB akisema kuwa Benki hiyo imekuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine hasa katika kubuni bidhaa bora ambazo zimekuwa zikikidhi mahitaji ya wateja mbalimbali ikiwamo wakina mama. “Kama tunavyojua serikali yetu imekuwa ikipambana kila kukicha katika kuwawezesha wanawake kutimiza malengo yao hususani katika shughuli za uzalishaji ambazo zimekuwa zikiwapatia kipato. Nafarijika sana ninapoona Benki ya CRDB ikiwa mmoja wa vinara wa kutimiza adhama hii ya serikali kupitia bidhaa na huduma zake” alisema Prof. Ndalichako. Waziri huyo pia aliishukuru Benki ya CRDB kwa msaada ambao wameutoa kwaajili ya ujenzi wa mabweni, alisema wizara itahakikisha msaada huo unafanya kazi ilikusudiwa na kuwaomba wadau wengine wa elimu nao wajitokeze katika kusaidia kuinua kiwango cha elimu nchini.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mama Stella Manyanya

Akifunga hafla hiyo Dkt. Kimei aliwasihi wakina mama wasiwe nyuma katika kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza kwani huo ndio msingi mkubwa wa kauli mbiu ya Jiwezeshe. “Ni lazima wakinamama wenyewe wawe na utayari kwa kujiwezesha kwanza. Kujiwezesha kunaweza kuwa ni kujiongezea elimu, kupata mafunzo mapya ya biashara au kuchangamkia fursa zipatikanazo katika taasisi za fedha ili kuanzisha au kupanua miradi yao na kufanikisha ndoto zao,” alisema Dkt. Kimei.

-MWISHO-

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tully Esther Mwambapa +255 769 200 600
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu +255 784 002020 This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Benki ya CRDB yatoa Msaada katika Makao ya Wazee na Walemavu wasiojiweza, Bukumbi, Mwanza.

Msaada
Mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB Dr. Charles Kimei, Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mh. Magesa Mulongo pamoja na Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli

Mwanza Tanzania, Marchi 05, 2015 – Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa vifaa vya kuzalishia umeme pamoja na chakula wenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 53, ikiwa ni moja ya sehemu ya Benki hiyo katika kuisaidia jamii. Kwa kuzingatia mahitaji ya jamii inayoizunguka, Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kusaidia jamii ambayo inalenga kurudisha kiasi cha asilimia moja ya faida ya Benki hiyo kila mwaka, ili ziende katika shughuli za kijamii, hususani katika nyanja za elimu, afya na mazingira.

Akizungumza katika makabidhiano hayo ambayo yalihudhuriwa na mke wa raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa mama Janet Magufuli pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Magesa Mulongo, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Benki ya CRDB inatambua changamoto mbalimbali wanazozipata wazee na walemavu wasiojiweza. Tunatambua kuwa taifa bora ni taifa ambalo linajali na kutambua mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa hilo. Pia tunatambua kuwa ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa wazee, walemavu na wasiojiweza katika jamii yetu wanapata matunzo stahiki.”

Akimnukuu muandishi na mtangazaji mahiri wa Kimarekani, Andy Rooney ambaye aliwahi kusema “the best classroom in the world is at the feet of an eldery person” akimaanisha kuwa mafundisho bora zaidi duniani yanapatikana kutoka kwa wazee wetu. Dkt Kimei alisema kutokana na usemi huo Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya jamii haina budi kujitoa katika kuwatunza, kuwalea na kuwaenzi wazee wetu ili kuiwezesha jamii na taifa kwa ujumla kuvuna busara zao.

Kituo cha wazee na walemavu wasiojiweza cha Bukumbi kilijengwa na kuanzishwa na serikali mwaka 1974 ili kusaidia kundi hilo maalum kwa kuwapatia matunzo na ulinzi. Toka kipindi hicho kituo hicho kimekua kikiendelea kutoa huduma kwa wazee wanaotoka sehemu mbalimbali za kanda ya ziwa. Kituo hicho kwa sasa kina jumla ya wakazi 108 ambapo kati yao wanawake ni 55 na wanaume 36 na kwa upande wa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ni 17 ikiwa wakike ni 10 na wakiume 7. Tokea kuanzishwa kwake kituo hicho kimekuwa kikiendeshwa na Serikali kupitia ustawi wa jamii lakini kutokana na changamoto mbalimbali kituo hicho kimekua kikitegemea zaidi misaada toka kwa wafadhili mbalimbali wakiwemo watu binafsi, mashirika ya misaada na taasisi za binafsi.

Msaada
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB akikabidhi sehemu ya msaada kwa Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli

Mapema mwaka huu mama Janeti Magufuli alitembelea kituoni hapo, ambapo uongozi wa kituo ulimuelezea changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakikumbana nazo. Mama Magufuli alichukua changamoto hizo na kuziwasilisha kwa ungozi wa Benki ya CRDB ikiiomba Benki hiyo kuweza kusaidia kutatua changamoto zinazokikumba kituo kicho. Akiongea katika hafla hiyo ya makabidhiano ya msaada huo mke wa raisi mama Janeti Magufuli aliishukuru na kuipongeza Benki ya CRDB kwa kuonyesha moyo wa kipekee katika kuwasaidia wazee na walemavu wasiojiweza katika kituo hicho cha Bukumbi.

Akiongea wakati wa makabidhiano ya msaada huo ambao ulijumuisha vifaa vya kuzalishia umeme wa jua “Solar panel”, mchele kilo 6000, unga kilo 6000, maharage kilo 3000, mafuta ya kupikia lita 1,000, Sukari kilo 2,500, madawa mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni mbili, vitu hivyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 53 za kitanzania. Dkt. Kimei alimpongeza mama Janet Magufuli kwa kujitoa kwake katika kutafuta suluhisho la changamoto nyingi zinazowakabili wakinamama, walemavu, wazee, watoto na wasiojiweza nchini. “Ama kwa hakika huu ni moyo wa kipekee, na naomba ni seme kweli taifa la Tanzania limepata mama mlezi anayewapenda na kuwajali watoto wake” alisema Dkt. Kimei.

Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa kituo hicho Mzee Bundala ambaye pia ni Mkuu wa kituo alisema uongozi wa kituo hicho pamoja na wakazi wake wote wamefarijika sana kwa msaada huo na wanaimani utaweza kutatua changamoto zao kwa kiasi kubwa sana. “Hakuna maneno yanayoweza kuonyesha furaha yetu, tunachoweza kusema ni tunashukuru sana na tunawaombea kwa Mungu pale mlipo toa basi akawaongezee maradufu.”

Katika hotuba yake fupi mama Janeti Magufuli pia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwajali na kuwathamini wanawake na kuwa benki ya kwanza nchini kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la “Malkia Akaunti,” huduma za bima kwaajili ya kina mama “Lady Jubilee” na mikopo maalum kwa ajili ya wanawake ijulikanayo kwa jina la “Mikopo ya Wafi”. Mama Magufuli alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakinamama kuweza kutumia fursa hizo zilizopo katika kukuza na kuendeleza biashara zao. “Wanawake sisi ndio nguzo ya familia hivyo fursa za akaunti za Malkia na mikopo ya WAFI ni muhimu kwa manufaa ya familia na taifa zima kwa ujumla” alisema mama Magufuli.

Dkt. Kimei alihitimisha hotuba hiyo fupi kwa kumuhakikishia mama Magufuli kuwa Benki hiyo ipo pamoja na wakina mama huku akimuomba kuwa balozi wa fursa hizo zinazopatikana ndani ya Benki ya CRDB kwa kuwafikishia ujumbe wa bidhaa na huduma hizo wakina mama pindi atapopata fursa ya kukutana nao.

-MWISHO-

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tully Esther Mwambapa
+255 769 200 600
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Godwin Semunyu
+255 784 002020
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

PRESS RELEASE: Benki ya CRDB yazindua maadhimisho ya sherehe za miaka 20 toka kuanzishwa kwake,

Dar Es Salaam Tanzania, Februari 17, 2016– Benki ya CRDB imezindua sherehe za maadhimisho ya miaka ishirini ya benki hiyo katika hoteli ya Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema, “Mwaka huu Benki ya CRDB inaadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwake hivyo basi tumeona ni vyema tukasherehekea mafanikio tuliyoyapata ndani ya kipindi hiki pamoja na wateja wetu. Sisi sote tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa benki ya CRDB hasa katika rasilimali, amana, mtandao wa matawi, mikopo na uchangiaji mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.”

Akielezea historia ya Benki ya CRDB, Dkt. Kimei alisema benki hiyo ilianzishwa tarehe 1 mwezi Julai mwaka 1996 kufuatia kutofanya vizuri kwa iliyokuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini iliyojulikana kama Cooperative Rural Development Bank. Dkt. Kimei alisema kuwa benki ilikabiliwa na matatizo mbalimbali katika uendeshaji wakati wa kuanzishwa kwake ikiwamo mfumo duni wa Tehama ambao ulileta changamoto kubwa hasa katika utunzaji wa mahesabu. Kutokana na mwanzo kuwa mgumu benki hiyo ilipata hasara ya jumla ya shilingi bilioni 1.8 mwaka uliofuatia yaani mwaka 1997. Baada ya mwaka huo benki ilijipanga vizuri na imekuwa ikiendelea kupata faida mwaka hadi mwaka na kukua na kustawi hadi kufikia kuwa benki inayoongoza Tanzania.

Dkt. Kimei alisema hadi kufikia Desemba 2015 Benki ya CRDB imekua maradufu kutoka matawi 19 yaliyokuwa na jumla ya wafanyakazi 400 wakati ilipoanzishwa hadi kufikia matawi 198 na jumla ya wafanyakazi 2,682, huku idadi ya wateja ikiongezeka hadi kufikia 1,800,000 kutoka 120,000 ambao benki ilianza nao. “Ama hakika tumepiga hatua kubwa sana ukilinganisha na pale tulipoanzia kwani pamoja na mafanikio hayo, vilevile amana za benki zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 40 hadi shilingi trilioni 4.2, mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 2 hadi kufikia shilingi trilioni 3.3, wakati jumla ya Rasilimali imeongezeka kutoka shilingi bilioni 54 hadi kufikia shilingi trilioni 5.4,” alisema.

Benki ya CRDB imekuwa ikisifika kwa kuongoza kwa ubunifu wa bidhaa na huduma mbambali ikilenga kuwahudumia wateja wake vizuri zaidi na kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla. Ikiienenda sambamba na kauli mbiu yake ambayo imejielekeza katika kuwajali wateja “Benki ninayomsikiliza mteja,” Benki ya CRDB ndio iliyokuwa benki ya kwanza Tanzania kuingiza sokoni Mfumo wa Malipo kwa kutumia Kadi (TemboCard), Mashine maalumu za kuwekea fedha (ATMs), Huduma za benki kupitia simu ya mkononi (SimBanking), Matawi yanayo tembea, Vifaa maalumu vya kulipia manunuzi (PoS), Huduma za kibenki kupitia mtandao (Internet Banking), Kituo cha Huduma kwa Wateja, huduma za biashara kupitia mtandao wa intanenti, Huduma kupitia madawati ya kimataifa ya China na Indian Desk, na huduma za kibenki kupitia mawakala (FahariHuduma Wakala) ambao sasa wamefikisha mawakala 1,769 nchi nzima.

read more

Dkt. Kimei alisema kuwa katika ukuaji huu wa Benki ya CRDB, pia wamefanikiwa kuanzisha kampuni mbili tanzu za “CRDB Bank Microfinance” inayojihusisha na biashara na mikopo kwa wakulima na wafanyabishara wadogo wadogo na CRDB Bank-Burundi ambayo imefunguliwa nchini Burundi ili kujenga daraja la kibiashara kati ya nchi hizi mbili. Kampuni hizo zimeongeza chachu kubwa katika ukuaji wa biashara ya benki hiyo pamoja na kuiletea umaarufu katika nchi za kanda ya afrika ya mashariki na kati.

Akizungumza kuhusu mchango wa benki hiyo katika maendeleo na ustawi wa jamii Dkt. Kimei alisema, “Benki ya CRDB imejiwekea sera maalum ya kuchangia kwenye mahitaji ya jamii ambapo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida yake ili itumike kusaidia katika maeneo ya elimu, afya na mazingira. Kwa mfano mwaka 2015 benki yetu ilitumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 katika kusaidia jamii inayoizunguka.”

Akielezea siri ya mafanikio hayo yaliyopatikana katika kipindi hicho, Dkt. Kimei alisema siri kubwa ni uwepo wa wafanyakazi wazuri, wenye kutii masharti yanayoendana na utamaduni wa biashara waliojiwekea, pamoja na kuwa wabunifu. Pia aliwashukuru wanahisa wa Benki hiyo kwa ushirikiano wanaotoa kwa uongozi wa Benki ambao umekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ambayo Benki imejiwekea. Katika mwendelezo wa shukrani zake Dkt. Kimei aliishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kiabashara ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa ustawi wa taasisi nyingi za kifedha nchini.

Dkt. Kimei alihitimisha kwa kuwashukuru wateja na wadau wengine wa Benki ya CRDB ambao kwa namna moja au nyingine wamechaingia kufanikisha mafanikio ya Benki hiyo huku akiwasihi waendelee kutumia bidhaa na huduma za Benki hiyo kwani Benki ya CRDB imejipanga vizuri katika kuboresha huduma na maisha ya wateja wake. Wadau mbalimbali waliohudhria katika uzinduzi wa maadhimisho ya sherehe hizo wamesema mafanikio haya makubwa iliyoipata Benki ya CRDB yanatokana uongozi bora wa wazawa na ubunifu wake kwenye bidhaa na huduma wanazotoa ambazo zimepelekea benki hiyo kutambulika, kuthaminiwa na kuwa chaguo nambari moja kwa wateja.

Benki ya CRDB imekuwa ikipata tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2004 benki hiyo ilipata tuzo ya ubora wa huduma ya “Euro Money” iliyotolewa na jumuiya ya mabenki barani ulaya. Benki pia imeweza kujitwalia tuzo ya umahili wa chapa yaani “Superbrand” kwa miaka mitano mfululizo toka mwaka 2010 na tuzo wa “Muajiri bora wa mwaka” inayotolewa na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE) kwa zaidi ya miaka sita mfululizo.

-MWISHO-

(function($){ $(document).on('ready', function() { }); })(jQuery);